Bwana Yesu asifiwe….
Biblia ni nini?
Biblia ni sauti ya Mungu iliyoifadhiwa kwenye maandishi. Sauti hii i hai hata leo ikifanya kazi ya kutufundisha,kutuonya makosa yetu,kutuongoza katika njia ipasayo kuiendea na kutuadabisha katika haki (2 Timotheo 3:16). Hivyo basi biblia ni makusanyo ya vitabu vitakatifu vilivyohifadhi sauti ya Mungu. Na kwa sababu biblia inatupa muongozo mzuri wa namna ya kumlingana Mungu kwanza kwa kumpokea Yesu Kristo,kupitia hilo na ndio maana wengine husema kwamba biblia ni katiba ya mbinguni.
Biblia ina mgawanyo wa maagano mawili,nayo ni;
- Agano la kale ( vitabu 39 )
- Agano jipya ( Vitabu 27)
A).AGANO LA KALE. (VITABU 39)
Neno“agano” ni mapatano/makubaliano ya kudumu baina ya watu wa pande mbili zaidi,au baina ya Mungu na watu wake. Makubaliano ya namna hii hayavunjwi kiwepesi kwa maana agano si mkataba. Kwa kuwa mkataba unaweza ukavunjwa,kuahirishwa au kuisha muda wake na kuandika mkataba mwingine. Agano hudumu kwa muda usiojulikana.
Bwana Mungu aliingia agano na wana wa Israeli,agano hili lilikuwa ni agano la kwanza lijulikanalo kuwa ni agano la kale. Akawapa sheria na maagizo 613 lakini mwishoe walilivunja kwa maana hawakuliweza.
“Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema BWANA. Yeremia 31:31-32
Sheria zilikuwa ni nyingi mno,hawakuweza kutembea katika sheria na magizo,na mausia na hukumu hizo zote.
HIVYO BASI TUNAJIFUNZA MAMBO YAFUATAYO KUPITIA AGANO LA KALE ;
- Agano la kale ni kivuli cha agano jipya (Wakolosai 2:17).
- Agano la kale linatazamia sadaka ya Kristo msalabani ( Mwanzo 3:15- tabiri ya kwanza ya ujio wa uzao wa mwanamke atakaye ukomboa ulimwengu na dhambi zake)
- Agano la kale limebeba ahadi ya ukombozi (ahadi juu ya umwagaji wa Roho mtakatifu Yoel 2:28,ahadi ya ukombozi,ahadi ya neno la Kristo)
- Agano la kale limebeba maelezo juu ya taifa la Israeli
- Agano la kale ni zamani za ujinga ambapo Mungu alifanya kama hazioni,hakukuwa na neema ya kutubu kama ilivyo agano jipya. ( Matendo 17:30)
- MTAZAMO KUHUSU VITABU 39 VYA AGANO LA KALE.
Agano la kale liliandikwa zaidi katika lugha ya Kiebrania lakini ikumbukwe kwamba katika uhamisho wa Babeli,lugha ya Kiaramu ndio lugha iliyotawala na maana baadhi ya mafungu ya maneno katika kitabu cha Ezra,Yeremia na Danieli yaliandikwa kwa lugha hiyo ya Kiaramu.
Katika vitabu hivi 39 viliandikwa kwa chanda cha Mungu akitumia watu maalumu aliowachagua na kuwavuvia uweza wake. Sasa vitabu hivi nimevigawa katika makundi matano,nayo ni;
01.Vitabu vya sheria; ( vitabu 5)
- Mwanzo.
- Kutoka.
- Mambo ya walawi.
- Hesabu
- Kumbu kumbu la torati
Maelezo mafupi;
Vitabu hivi hujulikana kuwa ni vitabu vya torati,au Pentateuko vyenye kueleza sheria yote alitoa Mungu kupitia Musa. Tena hujulikana kuwa ni vitabu vya Musa. Hivyo vifungu vingi katika Pentateuko (vitabu vitano)vinamtaja Musa kuwa anaiandika sheria na historia ya watu wa Israeli. Soma ( Kutoka 17:14,24:4,34:27,Hesabu 33:1-2,Kumb.31:9). Na hata waandishi wa baadae walieleza habari ya uandishi wa Musa Ezra 6:18 n.k.Yesu nae anazungumzia Torati kama kitabu cha Musa- (Marko 12:26),na sheria ya Musa soma Luka 24:44. Ukiwa msomaji mzuri utaona Yesu anasema ya kwamba Musa aliandika habari zake (za Yesu) soma Yoh.5:46-47
Vitabu hivi vitano vinatoa taswira halisi ya mwanzo wa kila kitu kama vile uanzapo kusoma kitabu cha mwanzo. Ni ukweli usiopingika kwamba kama unataka kujifunza neno la Mungu basi huda budi kuvisoma vitabu hivi.
02.Vitabu vya historia (Vitabu 12)
- Yoshua.
- Waamuzi.
- Ruthu.
- 1 Samweli.
- 2 Samweli.
- 1 Wafalme.
- 2 Wafalme.
- 1 Mambo ya nyakati.
- 2Mambo ya nyakati.
- Ezra.
- Nehemia.
- Esta.
Maelezo mafupi.
Yoshua alikuwa ni mwanafunzi wa Musa. Alipokufa Musa Yoshua akaongoza wana wa Israeli. Musa alimuandaa Yoshua ,na ndio maana mahali pengi ilimbidi Musa aongozane na Yoshua ikiwa ni mosa ya njia ya kufundisha kazi. Mfano Musa alipopanda mlimani kuchukua zile sheria kumi za Mungu,Musa alikuwa na Yoshua,ingawa Yoshua hakupanda mpaka kileleni soma Kutoka 32:17.
Kitabu cha Waamuzi;
Kitabu hiki cha Waamuzi kinachukua kipindi cha zaidi ya miaka mitatu,kipindi kati ya kifo cha Yoshua kama mwaka 1390 kk ( katika mlingano wa kutoka Misri ilikuwa 1446 kk) na kutawazwa mfalme Sauli kama mwaka 1028kk. Kipindi hiki,taifa lilipitia katika mateso. Ingawa kitabu hakisemi moja kwa moja ni nani hasa aliyekiandika lakini Samweli yeye mwamuzi wa mwisho wa Israeli pamoja na kina Nathani,na Gadi. ( 1 Nyakati 29:29) Samweli ndiye mwandishi.
Kitabu cha Ruthu
Ni moja ya kitabu kilichojaa simulizi zenye mafundisho mazuri yenye kumtumia muhusika mkuu Naomi. Kitabu hakielezi ni nani alikiandika lakini kulingana na masimulizi yake inaonesha ni mwanamke ndie mwandishi wa kitabu hiki.
Samweli wa kwanza na wa pili
Vitabu hivi viwili hapo kwanza kilikuwa ni kitabu kimoja. Hivyo vinaunda sehemu ya vitabu vya Waamuzi,Samweli na Wafalme. Vitabu hivi vina maelezo mazuri ya kihistoria ya Israeli. Kulingana na mapokeo ya Kiyahudi yanameonesha Samweli kuwa ndie mwandishi wa vitabu hivi. Hata hivyo sehemu za kitabu inawezekana ikawa imeandikwa na mtu mwingine kwa sababu baadhi ya matukio yaliyoandikwa yalitokea baada ya kifo chake Samweli ambapo kifo chake kimeandikwa katika 1 Samweli 25:1
1 na 2 Wafalme
Mwanzoni Wafalme kilikuwa ni kitabu kimoja,lakini kiligawanywa mara mbili kwa sababu kilikuwa kirefu sana Kiyunani ya Agano la kale iliyokuwa ikiitwa “Septuaginta” ,Samweli zote mbili ziliwekwa pamoja na Wafalme zote mbili chini ya kichwa cha habari cha milki au falme. Hivyo kulingana na mapokeo ya zamani yanaeleza kuwa Yeremia ndie mwandishi.
1 na 2 Mambo ya nyakati
Kitabu hiki kinatoa muhtasari mfupi wa agano la kale. Ndio maana baadhi ya wasomi husema mambo ya nyakati ni biblia ndani ya biblia kwa maana kinasimulia historia takatifu tangu uumbaji wa mwanadamu hadi kurudi uhamishoni Babeli . Mpaka sasa kitabu hiki hakijasema mwandishi ni nani haswa,lakini Ezra mwandishi anaonekana kuwa ndie mwandishi,hii imetokana na uhusiano uliopo kati ya kitabu cha Ezra na Nehemia kwa upande mmoja na Mambo ya nyakati kwa upande mwingine. Kwa maana hapo mwanzoni kulikuwa na mfanano/mkubaliano wa baadhi ya mambo.
03. Vitabu vya mashairi ( Vitabu 5)
- Ayubu.
- Zaburi.
- Mithali.
- Muhubiri.
- Wimbo uliobora.
Maelezo mafupi;
Kitabu cha Ayubu
hiki ni kitabu cha zamani sana lakini bado umuhimu wake hata leo upo. Tunajifunza mateso ya mwenye haki yakiwasilishwa na mtu aliyekuwa mkamilifu na mwelekevu wa moyo,Ayubu. Tunajinza kumbe kuna mateso ya mwenye haki yanayoruhusiwa na Mungu mwenyewe kwa lengo la kutuadabisha kama sehemu ya mtihani. Wasomi hawana uhakika ni lini na ni nani aliyekiandika.
Kitabu cha Zaburi
Daudi aliyeishi kati ya mwaka 1011 mpaka 941 kabla ya Kristo aliyekuwa kijana mchunga kondoo,mwanamziki,askari na mfalme aliandika Zaburi 73 kati ya Zab.150(3-9,11-32,34-41;51-65,68-70,86,101,103,108-110,122,124,138-145 )ikiwa Zaburi ya 2 na ya 95,ambazo kawaida hutazamwa kama Zaburi zisizo na mwandishi,lakini hata hivyo Daudi ndie aliyeziandika na hapo kuna mfanya Daudi ahusike na asilimia 50 ya Zaburi.
Yupo kuhani aitwae Asafu aliyeoongoza huduma ya muziki hekaluni,huyu alikusanya Zaburi kumi na mbili (50,73-83). Pia ushirika wa waimbaji watoto wa Kora walitunga Zaburi 11 zaidi (42-49,84,87). Lakini Zaburi mbili zinachukuliwa ni za Sulemani (72,127) hali Musa,Hemani na Ethani walichangia Zaburi moja kila mmoja (90,88 na 89) Zab.ya Musa iliandikwa wakati wa kuondoka Misri,na kukusanywa wakati wa Daudi. Kwa mlolongo huo,huacha Zaburi arobaini na saba ambazo waandishi wake hawajulikani.
Kitabu cha mithali,Muhubiri na wimbo ulio bora – Bila shaka muandishi anajitambulisha kwa matukio na maelezo yake mwanzoni mwa vitabu hivi kuwa alikuwa ni mtoto wa Daudi,Suleimani mfalme. Mapokeo ya wasomi yanasema kwamba Sulemani aliandika kitabu cha wimbo ulio bora katika ujana wake,Mithali katika utu uzima wake na Mhubiri katika uzee wake.
04.Manabii wakubwa (vitabu 5)
- Isaya.
- Yeremia.
- Maombolezo
- Ezekieli.
- Danieli
Maelezo mafupi.
Nabii Isaya – Aliishi nyakati za utawala wa uzia,Yothamu,Ahazi na Hezekia waliokuwa wafalme kipindi cha kati ya mwaka 767kk na 687 kk. Nabii huyu aliishi katika nyakati ngumu sana,si wengi wanaofahamu hivi kwa maana leo tusomapo tunaweza kufikiria kwamba mazingirayalikuwa mepesi,lah! Ulikuwa ni wakati mgumu kwa sababu miaka kama 150 taifa lilikuwa limegawanyika katika falme mbili yaani Israeli kwa upande wa Kaskazini na Yuda kwa upande wa kusini ( 1 Wafalme 12:1-24).
Nabii Yeremia-alizaliwa yapata mwaka 645 kk. Alitoka katika familia ya kikuhani iliyokuwa katika kijiji cha ANATHOTHI ( Yeremia 1:1) ( Si mbali sana na Yerusalemu,Anathothi ilikuwa kaskazini mwa Yerusalemu). Aliitwa katika utumishi akiwa kijana mdogo kama miaka kumi na minane hivi (Yeremia 1:2) yapata kama mwaka 627 kk.
Kitabu cha maombolezo – Kulingana na mapokeo,yaliyotunzwa katika tafsiri za Biblia ya kigiriki (Septuaginta) na ya Kilatini zinamtaja kuwa Yeremia ndie mwandishi. Bila shaka Maombolezo kiliandikwa muda mfupi baada ya 587 kk.
Kitabu cha Ezekieli – Nabii huyu mkubwa nae alitoka katika familia ya kikuhani soma Ezekieli 1:3. Jina la nabii huyu “Ezekieli ” lina maana ya “Mungu na aimarishe” au “ Mungu Yeye mwenye kuimarisha” Hivyo sawa sawa na jina lake Ezekieli,alikuwa ni nabii wa kuimalisha palipomomoka. Ezekieli alitawaliwa na Roho sana kiasi kwamba alikuwa akiona . Na kama ilivyokuwa hali ngumu kwa Isaya,ndivyo ilivyokuwa hali ngumu kwa Ezekieli maana kulikuwa na mtafaruku na mchafuko wa kisiasa na kijamii.
Kitabu cha Danieli – Kitabu cha Danieli kimekusanya pamoja historia ya Wayahudi na watu wa Mataifa toka karne ya saba kabla ya Kristo hadi mwisho wa historia ya binadamu. Mwanzoni kitabu hiki kiliandikwa kwa lugha mbili Sura ya 1:1-2,4a na sura ya 8-12 ziliandikwa kwa lugha ya Kiebrania. Sura za 2:4b-7:28 ziliandikwa kwa Kiaramayo. Danieli mwenyewe ndie anasema ya kuwa yeye ndie mwandishi Danieli 7:1,28,8:2,9;2,10:1-2 na 12:4
05. Manabii wa dogo.( 12)
Hosea,Yoeli,Amosi,Obadia,Yona,Mika,Nahumu,Habakuki,Sefania,Hagai Zekaria,Malaki
Maelezo mafupi.
Hosea – hiki ndicho kitabu cha kwanza cha manabii wadogo,na ukumbuke kwamba kundi hili la manabii wadogo halina maana kwamba ni manabii kweli wadogo wadogo,hapana. Bali wamewekwa kwenye kundi la manabii wadogo kwa sababu ya ufupi wa wa makusanyo ya vitabu vyao. Hosea alitabiri karibu miaka mia nne kabla ya kuzaliwa Kristo. Jina hili Hosea lina maana “ Mungu anayeokoa”
Yoeli – Lina maana “Yahweh ni Mungu” huyu Yoeli alikuwa ni nabii kutoka katika ufalme wa kusini mwa Yuda. Ingawa wataalamu wa mapokeo ya kimaandishi wanadai kuwa kitabu hiki kiliandikwa na zaidi ya mtu mmoja.
Amosi – Amosi alitoka katika ufalme wa kusini wa Yuda na hasa Tekoa ( soma Amosi 1:1a) kusini kabisa mwa Yerusalemu. Nae Amosi anaweka wazi juu ya tar. Ya unabii wake kwamba ni miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi (1:1b) inaonekana kuwa tetemeko hili lilikuwa ni tetemeko baya sana kutokea kipindi hicho maana hata Zekaria naye analitaja Zekaria 14:5
Hivyo kwa kufupisha, kutoka nabii wa mwisho Malaki hadi ujio wa Kristo yapata kama miaka 400. Kipindi hiki kinajulikana kuwa ni kipindi cha ukimya lakini si kimya tu maana kulikuwa na shughuli nyingi zikiendelea. Na kwa sababu Kristo alishatabiriwa watu walisubiri ujio wa Kristo.
B.AGANO JIPYA. ( VITABU 27)
Awali ya yote twapaswa kuyajua yafuatayo;
- Agano jipya ni taswira/picha halisi ya kusudi la Mungu kupitia Kristo Yesu.
- Agano jipya limejengwa juu ya kazi nzima ya Kristo iliyomalizika msalabani.
- Agano jipya ukombozi kamili umeshuka ulimwenguni. ( Yoh.3:16)
- Agano jipya ni utimilifu wa ahadi ( ujio wa Yesu,ujio wa Roho mtakatifu)
- Agano jipya ni ukombozi kamili msalabani.
- Agano jipya ni kipindi cha Neema,kila mmoja anapaswa kufikiria toba (2 Petro 3:9) na kumpokea Yesu Kristo awe Bwana na Mwokozi wa maisha yake.
- Kupitia agano jipya tunajifunza kwamba ujio wa Yesu ulikuwa ni kutuokoa kutoka dhambini kwa kukata shauri kumpokea Yesu Kristo na kuyafanya mapenzi ya Mungu. Sasa ingekuwa ni vigumu kuyatimiliza mapenzi ya Mungu pasipo kupata kielelezo. Ndio maana ilimbidi Yesu auvae mwili (Yoh.1:14) aje duniani tena azaliwe chini ya sheria yaani kwenye asili ya dhambi ( Wagalatia 4:5). Kumbe Yesu alikuwa mwanadamu asilimia mia (lakini hakutenda dhambi) pia alikuwa Mungu asilimia mia. Tuangalie jambo hili;
Yesu Mungu kamili “ Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.” 1 Yoh.5:20
Yesu mwanadamu kamili “ Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;“ 1 Timotheo 2:5-6
01. Injili ( Vitabu 4 )
- Mathayo
- Marko
- Luka
- Yohana.
Maelezo mafupi;
Injili tatu za kwanza zinafanana sana na zina maelezo yanayofanana,kwa sababu hiyo zimdpewa jina la “injili za sinoptiki” sabubu ya muonekano mmoja.Mathayo anajihusisha na mafundisho ya Yesu na mazingira yake ya kiyahudi. Marko anamuelezea Yesu kama mtumishi wa Mungu.Luka yeye anazingatia zaidi ubinadamu wa Yesu. Yohana anamfunua Yesu kuwa ni Mungu.
Mathayo;
Inawezekana iliandikwa kabla ya kubomolewa kwa hekalu mwaka 70 bk. Hata hivyo Mathayo alikuwa shahidi wa macho katika matukio mengi aliyoyaandika. Alikuwa ni mtosha ushuru,lakini Bwana alimuhitaji aache kazi hiyo na awe mtume . Mathayo anatufundisha kupokea wito mara moja pasipo kujuliza uliza,maana yeye alipoitwa mara moja aliacha vyote akafuata Yesu ( Mathayo 9:9). Mathayo anamuelezea Yesu kama mfalme,na inasadikika kitabu hiki kilikuwa ni cha tatu cha injili kuandikwa,yaani Marko,Luka kisha kuandikwa Mathayo na kumaliziwa na kitabu cha Yohana.
Marko;
Mwana injili huyu ajitokezi na kueleza uandishi wake. Hata hivyo kimapokeo amekuwa akihusishwa na uandishi,aliitwa Yohana Marko binamu wake Barnaba ( Wakoloosai 4:10). Yohana ni jina lake la kiyahudi na Marko ni jina lake la Kirumi. Marko ndio injili ya kwanza kuandikwa. Hata hivyo,injili ys Mathayo inasadikiwa kuwa na asilimia 90 ya injili ya Marko kwa kuwa huyu Marko alianza kuandika.
Luka ;
Aikuwa ni daktari msomi nayetajwa kama mara tatu katika agano jipya Paulo anamtaja kama “ Rafiki yetu mpendwa Luka na daktari ” Wakolosai 4:14 pia mjoli (Felemoni 24). Luka aliishi na Paulo,Luk alipofika alikutana na Marko. Huyu alikuwa msomi,hivyo basi alijaribu kutafiti kwa kina habari sahihi za Yesu,kiasha akaziandika. Hata hivyo aliandika kwa marefu zaidi kiasi kwamba vitabu vyake vikagawanywa,vikawa ni viwili. Yaani Injili ya Luka, na Matendo ya mitume.
Luka anamuandikia Theofilo akimtaka ajue habari sahihi za Yesu kwa maana Theofilo yeye hakuwa mkristo,bali ni kiongozi wa Serikali ya kirumi. Inawezekana Theofilo alihofu imani ya Kikristo akijua ni utawala mwingine wa kiserikali ujao kuwaondoa wao,na kumbe habari za ufalme wa Yexu hazikuwa hivyo. Luka hakuwa myahudi bali alikuwa mmataifa,myunani,mwandishi wa kihistoria kwa maana simulizi zake zilitwaliwa na matukio yenye kuonesha tar,au wakati watukio. Mfano Luka 2:1-2,3:1-3.
Je kwa nini zilikuwa injili nne? Na isiwe injili moja tu?
Bwana Mungu aliruhusu injili ziwe nne kwa sababu mwinjilisti angelikuwa ni mmoja asingeliweza kutoa picha kamili ya maisha ya Kristo. Mfano ukizisoma injili zote nne,anapata uhalisia wa Yesu alivyo. Angalia; Mathayo anamuelezea Yesu kama mfalme,Marko anamuelezea Yesu kama mtumishi wa Mungu,Luka anamuelezea Yesu kama mwanadamu akihusisha kuzaliwa kwake hata kufufuka kwake,na Yohana anauelezea Uungu wa Yesu.
Pia ni vyema panapokuwa watu wanne wenye kueleza kiutofauti habari za Yesu ili kukamilisha ushahidi tosha. Lakini jambo mmoja la ajabu ambalo wote wanne hawakuandika ni shughuli au kazi alizozifanya Yesu kati ya umri wa miaka 12 hadi 30 (yaani ile miaka 18 ya Yesu).
Yohana ;
Mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda. (Yoh.21:7). Wanazuoni wanasema kwamba Yohane ndie mwanafunzi wa pekee aliyeishi miaka mingi ya utumishi kuliko wenzake. Alikuwa rohoni sana.
02.Matendo ya mitume.
Hiki ni kitabu cha kipekee kinachosimulia matendo ya kanisaa la kwaanza na jinsi lilivyoeenea katika changamoto zote. Luka yeye aliyekuwa tabibu na mmoja wa wanafunzi wa Paulo ndie aliyeandika kitabu hiki. Dibaji ya injili ya Luka na hii ya matendo zinafanana kwa kumtaja mtu aitwae Theofilo Luka 1:1-4,na Matendo 1:1.
Ni kitabu cha muhimu sana kinachotoa wepesi kuelewa maandiko matakatifu ya agano jipya. Kinazungumzia kwa makini historia ya kanisa baada ya miaka 30 ya Yesu. Luka mwandishi yule tabibu,anafuatilia jinsi injili ilivyoenezwa kutoka Jerusalemu hadi Rumi akitaja nchi zaidi ya 32,miji 54,visiwa 9 na watu 95 kwa majina yao na maafisa wa serikali na watawala mbali mbali katika barua zake.
Kitabu hiki kinaeleza jinsi injili ilivyoenezwa kuanzia Yerusalemu,Uyahudi,Samaria na mwisho wa nchi ( Matendo 1:8) ;
•Yeresalemu-Sura 1-7 kuenea kwa injili.
•Samaria – 8-12 Kuenea kwa injili.
•Hata mwisho wa nchi(nchi yote)-13-28.
Lakini gafla kitabu kinaish,hii inawezekana mwandishi alikuwa akiandika kitabu kingine na hatimae akakosa muda wa kumalizia au akafa kabla ya kumalizia. Au inawezekana kiliendelezwa lakini Mungu akakataa yale maendelezo kama ilivyokuwa kwa Paulo mtume aliyeandika nyaraka nne kwa Wakorintho lakini nyaraka mbili tu ndizo zilizokubaliwa na mbili Bwana akazikataa.
04.Nyaraka za Paulo (13)
Warumi, 1 Wakorintho, 2 Wakorintho, Wagalatia, Waefeso,Wafilipi, Wakolosai, 1 Wathesalonike, 2 Wathesalonike, 1 Timotheo,2 Timotheo Tito, Filemoni.
05.Nyaraka nyingine (8)
Waebrania;
Bila shaka walaka huu uliandikwa kabla ya kuharibiwa kwa hekalu katika mwaka 70 kk,inawezekana ikawa kati ya 64 kk na 68 kk. Kitabu hiki kinawalenga wakristo Wayahudi ndio hao hao walioitwa waebrania. Lakini mpaka sasa kitabu hakitaji ni nani aliyekiandika,hata hivyo mapokeo ya zamani yanawataja Paulo,Barnaba,Luka,au Klementi wa Rumi. Hivyo muandishi anaonekana kwamba alilifahamu vyema agano la kale lakini pia alimfahamu vyema Timotheo-Soma Waebrania 13:23.
Barua nyingine ni Yakobo,1 Petro,2 Petro,1-3 Yohana,Yuda.
06.Ufunuo – mtume Yohana ndie mwandishi akiwa kisiwani Patmo akiwa katika roho.